Makumi ya waandamanaji watiwa nguvuni Kongo DR
Makumi ya watu wametiwa mbaroni kwa kushiriki maandamano yaliyopigwa marufuku na serikali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Pierre-Rombaut Mwanamputu, Msemaji wa Polisi ya Kongo DR amesema watu 34 wamekamatwa kufikia jana katika mji mkuu Kinshasa kwa kushiriki maandamano hayo yaliyopigwa marufuku. Hata hivyo amesema hana idadi ya waandamanaji wengine waliokamatwa katika sehemu nyingine za nchi.
Polisi ya Kongo DR ilitangaza kuwa, maandamano yaliyoitishwa na wapinzani wa serikali kote nchini kuanzia Jumatatu ya juzi hayataruhusiwa na kwamba maafisa usalama watatumia nguvu zote kutawanya mkusanyiko wowote wenye zaidi ya watu 10.
Chama kikuu cha upinzani cha UDPS katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kimevitaka vyama vyote vya upinzani kushiriki katika maandamano hayo yaliyopigwa marufuku.
Maandamano hayo yamefanyika baada ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kumteua Bruno Tshibala, mmoja wa viongozi wa upinzani kuwa Waziri Mkuu, licha ya wapinzani kutaka nafasi hiyo ichukuliwe na Felix Tshisekedi mwana wa kiume wa mwanasiasa mkongwe wa nchi hiyo marehemu Mzee Etienne Tshisekedi.