Jeshi la Somalia laua magaidi katika uwanja wa ndege Mogadishu
Jeshi la Somalia limewaua magaidi wawili walioonekana wakivurumisha mizinga kuelekea uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mogadishu mapema Jumapili.
Msemaji wa Meya wa Mogadishu, Abdifatah Omar Halane amesema magaidi wawili walikuwa wakiyfatua mizinga wakati walipouawa na punde baada ya hapo gari walimokuwa likaripuka.
Uwanja wa kimataifa wa ndege wa Mogadishi ni makao makuu ya mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa, balozi na pia kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.
Kundi la kigaidi la Al Shabab ambalo hutekeleza hujuma hizo mara kwa mara halijatoa taarifa yoyote. Magaidi wakufurishaji wa Al Shabab ambao wanafungamana na mtandao wa Al Qaeda wanalenga kuipindua serikali ya Somalia na kuanzisha utawala wao nchini humo.
Kundi hilo hutekeleza hujuma za mara kwa mara ndani ya Somalia na pia katika nchi jirani ya Kenya.
Mashambulizi haya ya kigaidi yanayoaminika kufanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni, Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo alitangaza kuwa nchi hiyo ni eneo la vita, huku akitoa siku 60 kwa wanamgambo wa al-Shabaab waweke silaha chini na wajisalimishe.