Wahajiri 9000 waokolewa katika bahari ya Mediterania mwishoni mwa wiki
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema idadi ya wakimbizi waliookolewa katika bahari ya Mediterania wakijaribu kuelekea barani Ulaya mwishoni mwa wiki imevunja rekodi.
Babar Baloch, Msemaji wa shirika hilo amesema wahajiri wapatao 9000 waliokolewa katika bahari ya Mediterania, kusini mwa Italia, eneo ambalo ni lango la wahajiri hao wa nchi za Afrika kuingia barani Ulaya.
Naye Leonard Doyle, Msemaji wa Shirika la Kimataifa la Wahajiri IOM amesema hali nzuri ya hewa katika msimu huu wa machipuo imesababisha wanaofanya biashara ya magendo ya binadamu kuzidisha mikakati yao ya kuwapelekea wahajiri hao barani Ulaya kupitia safari ya majini.
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, wahajiri zaidi ya 900 wamezama na kufa maji katika bahari ya Mediterania, wakiwa katika safari hatari za kujaribu kuelekea barani Ulaya.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) karibu wahajiri laki tano na 15 elfu wamevuka bahari ya Mediterrania na kuingia Ulaya tangu mwanzoni mwa mwaka huu pekee na karibu 36,000 wameokolewa wakiwa katika safari hizo hadi kufikia sasa.
Mwaka jana wahajiri zaidi ya 5000 hususan Wakiafrika walipoteza maisha kwa kuzama baharini katika bahari ya Mediterania wakielekea Ulaya.