Magaidi wa Al-Shabab wamuua afisa mwandamizi wa usalama wa taifa Somalia
(last modified Thu, 27 Apr 2017 16:00:32 GMT )
Apr 27, 2017 16:00 UTC
  • Magaidi wa Al-Shabab wamuua afisa mwandamizi wa usalama wa taifa Somalia

Watu wenye silaha wanaoaminika kuwa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabab wamemuua kwa kumpiga risasi afisa mwandamizi wa usalama wa taifa wa serikali ya Somalia mbele ya nyumba yake katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu.

Afisa huyo wa Intelijinsia ambaye amehusika katika utekelezaji wa operesheni za usalama dhidi ya kundi hilo la kigaidi alikuwa amekaa mbele ya nyumba yake bila ya walinzi wake wakati wanamgambo hao waliobeba bunduki walipompiga risasi na kumuua. Afisa wa Polisi Ibrahim Nur amethibitisha kuuawa kwa afisa huyo mwandamizi wa usalama.

Amesema, polisi na vikosi vya usalama vilifika baadaye eneo la tukio kufanya uchunguzi na kuwasaka wanamgambo hao. Ameongeza kuwa ilikuwa vigumu kuzuia mauaji hayo kwa sababu afisa huyo alikuwa hana walinzi wakati alipouliwa.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Al-Shabab ambalo linaendelea kufanya mashambulio ya utegaji mabomu licha ya kupoteza karibu ngome zake zote kwa vikosi vya kijeshi vya Umoja wa Afrika AMISOM vinavyoisaidia serikali ya Somalia limethibitisha kuhusika na shambulio hilo.

Vikosi vya AMISOM vikiwa katika doria

"Sisi ndio tuliohusika na mauaji ya jenerali wa usalama wa taifa aitwaye Mohamud Haji Ali", ameeleza Abdiasis Abu Musab, msemaji wa operesheni za kijeshi za kundi hilo alipowasiliana na vyombo vya habari.

Afisa wa Polisi Ibrahim Nur amethibitisha kuwa washambuliaji hao walitoweka baada ya shambulio hilo.

Mapema mwezi huu kundi la kigaidi la Al-Shabab lilitangaza kuwa lilihusika pia na shambulio la bomu lililotegwa garini ambalo lililenga maafisa waandamizi waliokuwa wakiondoka kwenye kituo kimoja cha jeshi mjini Mogadishu. Watu 15 waliuawa katika shambulio hilo.../

 

 

 

Tags