Waislamu Nigeria kuishtaki serikali kwa kupuuza agizo la koti
Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria imesema inajiandaa kwenda mahakamani kuishtaki serikali ya nchi hiyo kwa kupuuza agizo lililotolewa na Mahakama ya Federali la kumuachia huru kiongozi wao Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Taarifa ya uongozi wa harakati hiyo imesema viongozi wa vuguvugu hilo la Kiislamu hawana chaguo jingine ila kuifungulia mashtaka serikali, kwa kutotii hukumu iliyotolewa mwaka jana na Mahakama ya Federali ya nchi hiyo.
Sheikh Zakzaky alikamatwa na jeshi la Nigeria mwezi Disemba 2015 baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya na jeshi hilo, na tangu wakati huo hadi hivi sasa serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Muhammadu Buhari inaendelea kumshikilia kinyume cha sheria.
Tangu wakati huo, Waislamu nchini humo wamekuwa wakifanya maandamano ya amani katika mji mkuu Abuja, jimbo la Kaduna na miji kadhaa ya nchi hiyo ukiwemo wa Katsina, Bauchi, Gombe na Minna. Hata hivyo maandamano hayo mara kwa mara yamekuwa yakiingiliwa na polisi ambao huwa wanayasambaratisha kwa kuwarushia waandamanaji mabomu ya kutoa machozi na kuwamwagia maji ya kuwasha.
Licha ya muhula uliotolewa na Mahakama ya Federali kwa ajili ya kuachiliwa huru msomi na mwanaharakati huyo wa kidini kumalizika tarehe 16 Januari mwaka huu, lakini serikali haijatekeleza amri hiyo.
Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa tarehe Pili Disemba mwaka jana na mahakama hiyo, kitendo cha kuendelea kushikiliwa na serikali ya nchi hiyo Sheikh Zakzaky, mkewe na wanaharakati wengine wa Kishia ni kinyume cha sheria.