May 01, 2017 14:06 UTC
  • AU yaonyesha masikitiko yake makubwa juu ya kuendelea mapigano Sudan Kusini

Umoja wa Afrika umeonyesha wasi wasi wake mkubwa kutokana na hali mabaya nchini Sudan Kusini na kuendelea mapigano sambamba na mashambulizi dhidi ya raia wa kawaida.

Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika sambamba na kuonyesha wasi wasi wake juu ya kuongezeka migogoro ndani ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, amesisitiza kuwa, pande zote za mapigano huko Sudan Kusini zinatakiwa kusimamisha mara moja hatua zao za kijeshi.

Mauaji yanayojiri Sudan Kusini

Akisisitiza kuwa njia za kijeshi haziwezi kuhitimisha mgogoro wa sasa wa Sudan Kusini, Faki Mahamat amesema kwamba, pande zote za mapigano zinatakiwa kubeba dhima ya roho za raia wa nchi hiyo. Katika taarifa ya jana, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, karibu nusu ya jamii ya watu wa Sudan Kusini, inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kwamba, njaa ndio tishio kubwa kwa nchi hiyo. Kabla ya hapo pia tume ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa, licha ya Sudan Kusini kukabiliwa na migogoro mingi ya kisiasa, kibinaadamu na kiuchumi, lakini serikali ya Juba imejikita tu katika kununua silaha kwa ajili ya jeshi, vyombo vya usalama na kwa ajili ya makundi mengine ya wabeba silaha washirika wake.

Raia wa kawaida wakiuawa Sudan Kusini

Sudan Kusini ilitumbukia katika mapigano ya ndani mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir, kumtuhumu aliyekuwa makamu wake wa rais Riek Machar kwamba alipanga njama ya kutaka kumpindua madarakani. Hadi sasa maelfu ya watu wamekwishauawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na machafuko hayo.

Tags