May 02, 2017 16:33 UTC
  • UN yampongeza Muntari kwa kukosoa ubaguzi wa rangi uwanjani

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amempongeza Sulley Muntari, mchezaji wa klabu ya Pescara ya Italia kwa kuamua kuondoka uwanjani kulalamikia ubaguzi wa rangi dhidi yake.

Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN amesema kiungo huyo wa kati raia wa Ghana ni mfano wa kuigwa ambaye ametoa ari, motisha na wakati huohuo changamoto kwa watu wengi haswa kwa afisi hiyo ya Umoja wa Mataifa, kutokana na kitendo chake hicho.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Ganeva nchini Uswisi, afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amelitaka Shirikisho la Soka Duniani FIFA kuliangalia kwa makini suala la wachezaji kubaguliwa na kudhalilishwa kwa misingi ya rangi zao wakiwa uwanjani.

Muntari, aliondoka uwanjani baada ya refa kumpa kadi ya manjano, alipolalamika kuwa baadhi ya mashabiki wakiwemo watoto walimrushia cheche za maneno ya kibaguzi, wakati wa mechi ya Ligi ya Serie A kati ya timu yake na klabu ya Cagliari. Huku akionekana kukerwa na kitendo hicho cha ubaguzi, Sulley Muntari aliwakabili mashabiki wa klabu ya Cagliari na kufoka kwa sauti akisema "Hii ni rangu yangu!" huku akiashiria rangi ya mkono wake.  

Mchezaji wa zamani wa Manchester United alivyodhalilishwa na Suarez

Kiungo huyo wa zamani wa Ghana mwenye umri wa miaka 32, alimuomba refa Daniele Minelli asimamishe mechi hiyo ya Jumapili kutokana na kitendo hicho cha kibaguzi, ili kuonyesha mfano mwema kwa mashabiki. Hata hivyo refa huyo badala yake alimpa kadi ya manjano katika dakika ya 89, hatua iliyosababisha mchezaji huyo wa zamani ya timu Portsmouth na Sunderland kupinga kwa kuondoka uwanjani.

Hii sio mara ya kwanza kwa mchezaji wa Kiafrika kudhalilishwa na kukosewa adabu wakiwa uwanjani katika nchi za bara Ulaya. 

Tags