Ivory Coast yaiomba Iran iisaidie kuimarisha sekta ya uchukuzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i28870-ivory_coast_yaiomba_iran_iisaidie_kuimarisha_sekta_ya_uchukuzi
Waziri wa Uchukuzi wa Ivory Coast, Amadou Kone ameiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iisaidie nchi hiyo ya Kiafrika kuboresha mfumo wake wa uchukuzi wa umma.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 09, 2017 14:22 UTC
  • Ivory Coast yaiomba Iran iisaidie kuimarisha sekta ya uchukuzi

Waziri wa Uchukuzi wa Ivory Coast, Amadou Kone ameiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iisaidie nchi hiyo ya Kiafrika kuboresha mfumo wake wa uchukuzi wa umma.

Waziri wa Uchukuzi wa Ivory Coast alitoa wito huo jana Jumatatu, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mahdi Aghajafari, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika mji mkuu wa kibiashara wa Kodivaa, Abidjan.

Amadou aliashiria kuhusu mpango wa nchi hiyo wa kuboresha sekta yake ya usafiri kufikia mwaka 2020, akisema kwamba taifa hilo linahitaji magari mepesi na mazito 50,000 kwa ajili ya kuimarisha uchukuzi nchini humo. Waziri wa Uchukuzi wa Ivory Coast ameiomba Iran iisaidie nchi hiyo kufikia ruwaza yake hiyo.

Kwa upande wake, Mahdi Aghajafari, Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema makampuni ya kutengeneza magari ya Iran yako tayari kuisaidia Kodivaa kufikia malengo yake hayo ya kuimarisha sekta ya uchukuzi.

Bendera za Iran na Kodivaa

Kadhalika wawili hao wamesisitizia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili za Iran na Kodivaa, haswa kwa Jamhuri ya Kiislamu kuisaidia nchi hiyo katika nyuga za ujenzi wa barabara, bandari na viwanja vya ndege.

Oktoba mwaka jana, Rais Hassan Rouhani wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Abdullah Mabri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ivory Coast hapa Tehran ambapo wawili hao waliashiria kuhusu mkondo wa ustawi wa uhusiano wa nchi hizi mbili. Rais Rouhani alisisitiza kuwa, Iran iko tayari kuimarisha uhusiano wake na Ivory Coast katika nyanja zote hasa katika sekta za kiuchumi.