Wanajeshi 3 wauawa wakitegua bomu nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29212-wanajeshi_3_wauawa_wakitegua_bomu_nchini_somalia
Kwa akali askari watatu wa jeshi la Somalia wamepoteza maisha baada ya mabomu yaliyokuwa yametegwa ndani ya gari moja lililokamatwa na maafisa usalama kuwalipukia katika mji mkuu Mogadishu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 17, 2017 13:54 UTC
  • Wanajeshi 3 wauawa wakitegua bomu nchini Somalia

Kwa akali askari watatu wa jeshi la Somalia wamepoteza maisha baada ya mabomu yaliyokuwa yametegwa ndani ya gari moja lililokamatwa na maafisa usalama kuwalipukia katika mji mkuu Mogadishu.

Meja Mohamed Hussein, afisa wa polisi wa ngazi za juu nchini humo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa waliouawa ni askari wataalamu wa kutegua mabomu. 

Amesema maafisa hao waliitwa kutegeua mabomu na mada za mlipuko zilizokuwa zimesheheni ndani ya gari moja lililonaswa na maafisa usalama katika wilaya ya Wadajir.

Abdiasis Abu Musabi, Msemaji wa genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab amekiri kuwa kundi hilo lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda limehusika na hujuma hiyo ya kigaidi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Magaidi wa kitakfiri wa al-Shabaab wa Somalia

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa Somalia kuiomba jamii ya kimataifa iisaidie nchi yake katika kupambana na ugaidi, ufisadi na umaskini wa kuchupa mipaka; mambo ambayo alisema ni adui mkuu wa nchi hiyo.

Rais wa Somalia aliyasema hayo katika mkutano wa kimataifa kuhusu Somalia uliofanyika hivi karibuni mjini London Uingereza kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Mkutano huo ulitanguliwa na msamaha wa siku 60 uliotangazwa na Rais Farmajo kwa wanachama wa al-Shabaab watakaoweka silaha chini na kujisalimisha.