Ubelgiji yaitaka serikali ya Burundi izungumze na wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2929-ubelgiji_yaitaka_serikali_ya_burundi_izungumze_na_wapinzani
Serikali ya Ubelgiji imeitaka serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi iandae mazingire ya kufanyika mazungumzo kati yake na wapinzani na kusisitiza kuwa udharura wa kufanyika mazungumzo hayo hivi sasa ni mkubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 12, 2016 11:56 UTC
  • Ubelgiji yaitaka serikali ya Burundi izungumze na wapinzani

Serikali ya Ubelgiji imeitaka serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi iandae mazingire ya kufanyika mazungumzo kati yake na wapinzani na kusisitiza kuwa udharura wa kufanyika mazungumzo hayo hivi sasa ni mkubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Mtandao wa habari wa Africa Time umeinukuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Ubelgiji ikisema katika taarifa yake iliyoitoa baada ya mazungumzo kati ya Didier Reynders, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo na mwenzake wa Burundi, Alain-Aimé Nyamitwe mjini Brussels, kwamba kuna udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya serikali ya Bujumbura na wapinzani.

Katika taarifa hiyo, serikali ya Ubelgiji imesema ina wasiwasi na hali ilivyo hivi sasa nchini Burundi na kusisitiza kuwa, kuna udharura wa kuandaliwa mazingira ya kufanyika mazungumzo haraka iwezekanavyo baina ya serikali ya Burundi na wapinzani kwa ajili ya kutoka kwenye mgogoro huo.

Aidha serikali ya Ubelgiji imepokea vizuri mpango wa kutumwa askari 200 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Burundi na kusema kuwa, wajumbe wa Umoja wa Ulaya wana matumaini kuwa hali ya haki za binadamu itaboreka nchini Burundi.

Burundi imetumbukia kwenye mgogoro wa ndani tangu takriban mwaka mmoja nyuma, yaani kuanzia mwezi Aprili 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumteua Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa mara ya tatu mfululizo nchini humo.