Unicef yatahadharisha kuenea kipindupindu Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29518-unicef_yatahadharisha_kuenea_kipindupindu_mashariki_ya_kati_kaskazini_mwa_afrika
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuwa, mamilioni ya watoto wa maeneo ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika wamo hatarini kutokana na uwezekano wa kuenea janga hatari la kipindupindu katika maeneo hayo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 24, 2017 14:22 UTC
  • Unicef yatahadharisha kuenea kipindupindu Mashariki ya Kati, Kaskazini mwa Afrika

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuwa, mamilioni ya watoto wa maeneo ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika wamo hatarini kutokana na uwezekano wa kuenea janga hatari la kipindupindu katika maeneo hayo.

Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo na kuinukuu UNICEF ikisema katika tamko lake la leo Jumatano kuwa, mapigano na ugonjwa wa kipindupindu unahatarisha afya ya watoto milioni 24 wa Yemen, Syria, Ukanda wa Ghaza, Iraq, Libya na Sudan.

Taarifa ya UNICEF imesisitiza kuwa, pande zinazopigana katika maeneo hayo zinapaswa kuacha mara moja kushambulia vituo vya afya na matibabu.

Vile vile imesema, sababu ya kuenea ugonjwa wa kipindupindu kwenye maeneo hayo ni kukosekana maji salama ya kunywa, kutokuwepo huduma nzuri za matibabu na kuongezeka mapigano siku baada ya siku.