May 31, 2017 15:00 UTC
  • Maafisa polisi 7, raia 1 wauawa katika shambulizi la bomu Lamu, Kenya

Maafisa saba wa polisi ya utawala wameuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa kando ya barabara katika kaunti ya Lamu, kusini mashariki mwa Kenya.

Noah Mwavanda, afisa mwandamizi wa timu ya usalama katika kaunti ya Lamu amesema, gari hilo lilikuwa linatoka eneo la Baure likielekea Mokowe wakati lilipokanyaga bomu na kuripuka.

Kadhalika raia mmoja ameuawa katika mripuko huo, ingawaje haijabainika iwapo alikuwa ndani ya gari hilo au kando ya barabara palipotokea mripuko huo.

Eneo la Baure liko karibu na Mpeketoni, mji ambao ulishambuliwa na genge la kigaidi al al-Shabaab mwezi Juni 2014, na kuepelekea watu 60 kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Hujuma ya wiki iliyopita iliyoua maafisa watano wa polisi Mandera, Kenya

Wiki iliyopita, maafisa usalama 14 wa Kenya waliuawa katika mashambulizi tofauti ya bomu na mada za miripuko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Wimbi hili la mashambulizi dhidi ya maafisa usalama nchini Kenya linajiri katika hali ambayo, hivi karibuni, Joseph Boinnet, Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo alitahadharisha kuwa baadhi ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wamejipenyeza nchini humo kutokea Somalia, kwa ajili ya kuvuruga usalama wa Kenya na kuwataka wananchi kuwa macho na kuripoti kwa vyombo husika, matukio yoyote wanayohisi yanaweza kuhatarisha usalama wa taifa.

Tags