Rais Salva Kiir akosa kuhudhuria mkutano wa IGAD kuhusu nchi yake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30374-rais_salva_kiir_akosa_kuhudhuria_mkutano_wa_igad_kuhusu_nchi_yake
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amekosa kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) unaofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa unajadili mgogoro wa wakimbizi katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 12, 2017 09:28 UTC
  • Rais Salva Kiir akosa kuhudhuria mkutano wa IGAD kuhusu nchi yake

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amekosa kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) unaofanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa unajadili mgogoro wa wakimbizi katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Marais na viongozi wa jumuiya ya IGAD, chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, wameeleza kusikitishwa kwao na hatua ya Rais Kiir kususia mkutano huo muhimu licha ya kualikwa na badala yake amemtuma Makamu wake aliyemteua Taban Deng Gai.

Mkutano huo unajadili kadhia muhimu ya mamilioni ya wakimbizi wa ndani na nje wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, akthari yao wakikabiliwa na baa la njaa. Zaidi ya raia 375,000 wa Sudan Kusini, asilimia 90 wakiwa ni wanawake na watoto, wamekimbilia Sudan tokea vita vya ndani vianze katika nchi yao mwaka 2013. Uganda nayo ina wakimbizi 883,000 kutoka Sudan Kusini huku wengine wakikimbilia nchi jirani ya Kenya.

 

Kiir na makamu wake wa zamani Machar

Baada ya mkutano wa IGAD uliofanyika mwishoni mwa mwezi uliopita wa Mei katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar ambaye kwa sasa anaripotiwa kuwa Afrika Kusini alisema kuwa, ni jambo la kusikitisha kuiona IGAD inampuuza na kukosa kumshirikisha kikamilifu katika mchakato wa amani na kurejesha utulivu nchini Sudan Kusini.

Hivi karibuni Kiir alitangaza kuwa, taifa hilo changa zaidi barani Afrika litafanya uchaguzi mwaka ujao 2018, baada ya kumalizika kipindi hiki cha mpito.