Magaidi wa Al Shabab waua watu 17 Mogadishu
(last modified Thu, 15 Jun 2017 07:14:12 GMT )
Jun 15, 2017 07:14 UTC
  • Magaidi wa Al Shabab waua watu 17 Mogadishu

Magaidi wa kundi la Al Shabab nchini Somalia wamewaua watu 17 katika hoteli moja katika mji mkuu Mogadishu.

Maafisa wa usalama wanasema magaidi waligongesha gari lilokuwa limesheheni mabomu katika hoteli ya kifahari ya Posh jana Jumatano na kisha kuvamia mgahawa wa Pizza House pembizoni mwa hoteli hiyo.

Taarifa zinasema magaidi hao walikuwa wamechukua mateka watu 10 katika mgahawa huo kabla ya kuokolewa na maafisa wa usalama.

Aidha maafisa wa usalama wamesema magaidi wawili wameuawa na hadi kufikia Alhamisi asubuhi duru zilikuwa zinadokeza kuwa baadhi ya magaidi bado walikuwa wamejificha ndani ya jengo hilo. Magaidi hao walikuwa wamevalia sare za kijeshi wakati wa hujuma hiyo.

Kati ya waliouawa ni raia mmoja wa Syria huku wafanyakazi Wahindi, Waethiopia na Wakenya wakiokolewa baada ya kutekwa nyara na magaidi.

Umoja wa Afrika umetuma kikosi chake katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. Kikosi hicho cha AMISOM kina wanajeshi kutoka Uganda, Kenya, Burundi na Ethiopia. Askari zaidi ya 22 elfu wanaunda kikosi hicho cha AU kwa ajili ya kupambana na kundi la al Shabab huko Somalia.

Ingawa kundi la al Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado lina wanamgambo wake katika baadhi ya vijiji na miji na hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa Serikali.

Tags