Maelfu ya wapiganaji wa Kiafrika wapo Libya
Taasisi ya Kuchunguza Silaha Nyepesi yenye makao yake mjini Geneva Uswisi imesisitiza kuwa maelfu ya wapiganaji wa Kiafrika wanapigana bega kwa bega na makundi mbalimbali yenye silaha nchini Libya.
Taasisi hiyo imesema katika ripoti yake kuwa, kushindwa kufikiwa makubaliano ya amani ya kutatua mizozo huko Chad, Darfur, Sudan na Niger kumetoa mwanya kwa wanamgambo kuingia Libya kupitia mipaka ya nchi hizo.
Taasisi ya Kuchunguza Silaha Nyepesi ya huko Geneva imeashiria pia kuwepo maelfu ya wanamgambo wa Afrika nchini Libya; na kusema kwamba, pande mbalimbali zinazozozana nchini humo zinawatumia wapiganaji hao vitani.
Hii ni katika hali ambayo makundi mbalimbali yanayozozana huko Libya yanatuhumiana yenyewe kwa yenyewe kuwa yanawatumia wapiganaji hao. Idadi ya wapiganaji hao imekuwa ikiongezeka mno nchini Libya tangu mwaka 2011.
Libya ilitumbukia katika machafuko tangu Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) ulipoingia kijeshi nchini humo mwaka 2011 katika kampeni za kumpindua kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi.