Magaidi wa Al Shabab wateka mji wa Garad, Somalia
Magaidi wa Al Shabab wameuteka mji wa bandarini wa Garad katika eneo la Puntland lenye mamlaka ya ndani Somalia.
Kundi hilo la magaidi wakufurishaji wenye mfungamano na mtandao wa Al Qaeda walichukua udhibiti wa mji huo Jumatatu baada ya kuushambulia kupitia idadi kubwa ya wapiganaji waliofika hapo kwa boti kadhaa.
Mkuu wa eneo la Garda Abdinur Abdullahi alisema magaidi wa Al Shabab waliingia mjini humo na kuwaambia wazee wa eneo hilo kuwa wataendelea kuteka maeneo zaidi na kukabiliana na wale wanaopinga sera zao.
Eneo la Puntland liko kaskazini mashariki mwa Somalia na mwaka 1998 lilijitangazia mamlaka ya ndani lakini lingali chini ya usimamizi wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia. Eneo hilo linapakana na eneo la Somaliland ambalo lilijitangazia uhuru mwaka 1991 baada ya kuangushwa utawala wa dikteta Siad Barre. Uhuru wa Somaliland hautambuliwi kimataifia. Puntland iko nje ya eneo la oparesheni za Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Afrika Somalia AMISOM venye askari 22,000 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.