Nyaraka mpya zafichua nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31196-nyaraka_mpya_zafichua_nafasi_ya_ufaransa_katika_mauaji_ya_kimbari_ya_rwanda
Nyaraka mpya za kihistoria zilizochapishwa hivi karibuni kwa mara nyingine tena zimethibitisha nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda baada ya kupita miaka 23 tangu kutekelezwa mauaji hayo.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jul 01, 2017 08:35 UTC
  • Nyaraka mpya zafichua nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda

Nyaraka mpya za kihistoria zilizochapishwa hivi karibuni kwa mara nyingine tena zimethibitisha nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda baada ya kupita miaka 23 tangu kutekelezwa mauaji hayo.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, imebainika kuwa Ikulu ya Rais wa Ufaransa, Élysée iliwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa Rwanda wakati huo kuwapatia silaha watekelezaji wa mauaji ya kimbari mwaka 1994. Amri hiyo ilitolewa wakati Rwanda ikiwa chini ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa. 

Mauaji hayo ya kimbari ya Rwanda ambayo yanatambulika kuwa ndiyo mauaji makubwa zaidi ya halaiki ya karne, yalipelekea kuuliwa raia zaidi ya laki nane katika kipindi cha siku 100. Hata kama chanzo cha mauaji hayo kinatajwa kuwa ni hitilafu zilizokuwepo kati ya makabila ya Wahutu na Watutsi, lakini mkono wa nchi za Magharibi kama Ufaransa na Ubelgiji pia unashuhudiwa pakubwa katika mauaji hayo ya kimbari. 

Arana Pare, mwanahistora na mhadhiri raia wa Burkina Faso ambaye pia ni mwanachama wa Taasisi ya Kirafiki na Mshikamano ya Mataifa ya Afrika amesisitiza kuhusu ripoti inayochunguza nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda kwamba, "kutolewa amri kama hiyo na Ufaransa su jambo la kushangaza kwa sababu, serikali ya Paris imekuwa ikisema uwongo na kukanyaga haki za mataifa ya Kiafrika ili kuimarisha nafasi yake na kueneza siasa zake za ukoloni mamboleo barani Afrika". 

Mauaji ya kimbari yalitokea nchini Rwanda mwaka 1994. Mauaji na mapigano ya ndani yalianza nchi humo baada ya kuangushwa ndege iliyokwua imembeba Rais Juvenal Habyarimana wa nchi hiyo karibu na uwanja wa ndege wa Kigali. Wanamgambo wa Kihutu wenye misimamo ya kufurutu ada walikituhumu chama cha wapiganaji wa Kitutsi cha RPF kuwa kilihusika na utunguaji wa ndege hiyo na wakaanzisha mauaji ya kimbari yaliyoratibiwa dhidi ya Watutsi.  

Wahutu wa Rwanda waliokuwa wakiwauwa Watutsi kwa mapanga 

Maelfu ya watu waliuawa na mamia ya wanawake wa Kitutsi walikamatwa mateka na kufanywa watumwa wa ngono katika mauaji hayo ya kimbari. Mauaji hayo yalijiri huku jamii ya kimataifa ikinyamaza kimya bila ya kuchua hatua zozote. Umoja wa Mataifa na Ubelgiji licha ya kuwa zilikuwa na wanajeshi huko Rwanda, lakini hazikuchukua hatua ya kusitisha mauaji hayo. Wanajeshi wa Ubelgiji na askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa pia baadaye waliamua kuondoka Rwanda baada ya askari wao kadhaa kuuawa. Ufaransa ambayo ilikuwa nchi muitifaki wa serikali ya Kihutu ya Rwanda wakati huo, ilituma wanajeshi nchini humo kwa ajili eti ya kutenga eneo salama la amani. Hata hivyo Ufaransa nayo inatuhumiwa kuwa si tu kwamba haikufanya jitihada za kutosha kusitisha mauaji hayo yaliyowalenga Watutsi, bali ilikuwa na nafasi kubwa katika mauaji hayo. Kiasi kwamba, Rais wa sasa wa Rwanda, Paul Kagame kwa mara kadhaa ameituhumu Paris kuwa ilihusika katika mauaji hayo ya kimbari, tuhuma ambazo zimekanushwa na Ufaransa. 

Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika doria nchini Rwanda mwaka 1994 huku wakiwapisha wanamgambo wa Kihutu 

Ufaransa inatuhumiwa kuhusika katika mauaji hayo ya Rwanda katika hali ambayo, ni miaka kadhaa sasa ambapo nchi hiyo inaendeleza siasa zake za kikoloni katika nchi mbalimbali barani Afrika. Ukweli ni kuwa Ufaransa imekuwa ikilihesabu bara la Afrika kuwa uchochoro wake wa kujinufaisha kwa maliasili na nguvu kazi ya nchi za bara hilo. Kuhusiana na suala hilo, tunaweza kuashiria uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi mbalimbali za bara hilo kama huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na kwingineko.

Kufichuliwa nyaraka mpya za kihistoria kuhusu nafasi ya Ufaransa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda kumezidi kuweka wazi mienendo ya kikoloni na siasa za uingiliaji kazi zinazotekelezwa na Ufaransa barani Afrika.