Kuakhirishwa mazungumzo ya usalama kati ya Sudan na Sudan Kusini
Mazungumzo ya amani kati ya Sudan na Sudan Kusini yameakhirishwa hadi wakati mwingine kutokana na matatizo ya kilojistiki.
Mawien Makol Arik, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan Kusini alisema jana Jumatatu bila ya kuashiria aina ya matatizo ya kilojistiki yaliyojitokea katika mazungumzo ya wiki hii kati ya viongozi wa kisiasa na kiusalama wa nchi mbili hizo na wala hakutaja wakati hasa wa kufanyika mazungumzo mengine. Hata hivyo amesema: Masuala kama uungaji mkono wa Sudan na Sudan Kusini waasi wa pande mbili katika maeneo ya mipaka yatachunguzwa katika mazungumzo yajayo.
Baada ya kupita miaka miwili, hatimaye viongozi wa Sudan na Sudan Kusini tarehe Pili Mei mwaka huu walikubaliana kuhusu mpango wa usuluhishi wa Umoja wa Afrika ili kukomesha uhasama na mzozo kati yao na kuanza tena mazungumzo ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiusalama na kijeshi kati ya nchi mbili hizo haraka iwezekakanvyo baada ya Sikukuu ya Idul Fitr.
Nchi mbili hizo zilikumbwa na hitilafu tangu mwaka 2011 kufuatia pande hizo kushindwa kutekeleza ipasavyo makubaliano ya amani. Sudan na Sudan Kusini pia bado zimeshindwa kufikia muafaka kuhusu namna ya kuondoa wanajeshi wao katika maeneo ya mipaka yanayozozaniwa.