UN yatahadharisha kuhusu ukosefu wa amani Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i31372-un_yatahadharisha_kuhusu_ukosefu_wa_amani_sudan_kusini
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini umetangaza kuwa nchini hiyo inasumbuliwa na hali hatari sana ya ukosefu wa amani.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jul 05, 2017 14:32 UTC
  • UN yatahadharisha kuhusu ukosefu wa amani Sudan Kusini

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini umetangaza kuwa nchini hiyo inasumbuliwa na hali hatari sana ya ukosefu wa amani.

Taarifa iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imesema kuwa, zaidi ya wafanyakazi 80 waliokuwa wakitoa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Sudan Kusini wametekwa nyara na makundi yenye silaha na kuuawa. 

Taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, mamilioni ya raia wa Sudan Kusini pia wamelazimika kukimbia makazi na nyumba zao kutokana mapigano na vita vya ndani. 

Maelfu ya watu wameuawa Sudan Kusini kutokana na machafuko ya ndani

Wakati huo huo Idara ya Takwimu ya Taifa ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, hali ya kibinadamu katika nchi hiyo imekuwa mbaya zaidi hatua kwa hatua tangu mwaka 2011 na kwamba wakati mwingine imekuwa mbaya zaidi kuliko ile ya Somalia, nchi inayotambuliwa kuwa na machafuko zaidi kuliko zote duniani.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 baada ya miaka mingi ya vita vya ndani na mwaka 2013 ilitumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya jeshi linalomuunga mkono Rais Salva Kiir na wafuasi wa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.