Jose Maria Aranaz: Kumefanyika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32356-jose_maria_aranaz_kumefanyika_ukiukaji_mkubwa_wa_haki_za_binadamu_drc
Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, kumeripotiwa kesi nyingi za ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kiafrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2017 23:18 UTC
  • Jose Maria Aranaz: Kumefanyika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu DRC

Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, kumeripotiwa kesi nyingi za ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Jose Maria Aranaz amesema kuwa, jumla ya kesi 2800 za ukiukaji wa haki za binadamu zimeripotiwa nchini humo tangu ulipoanza mwaka huu wa 2017 hadi mwezi huu wa Julai.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, kumesajiliwa kesi 884 za mauaji katika maeneo ambayo zinashuhudiwa vurugu na machafuko huku watu 230 wakiwa wahanga wa utumiaji mabavu wa kijinsia.

Maiti zilizopatikana katika makaburi ya umati mkoani Kasai katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza kuwa, wanajeshi 104 na polisi 20 wa nchi hiyo waliopatikana na hatia ya kukiuka haki za binadamu wameshtakiwa na kuhukumiwa adhabu mbalimbali katika kipindi cha miezi sita ya awali ya mwaka huu.

Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amewateua wataalamu watatu wa kimataifa watakaokuwa na jukumu la kufanya uchunguzi kuhusu vitendo vya utumiaji mabavu, ubakaji na ukiukwaji wa haki za binadamu katika mkoa wa Kasai.

Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kuwa, timu hiyo ya uchunguzi itaongozwa na Bacre Ndiaye raia wa Senegal, Luc Côté wa Canada na Fatimata M'Baye raia wa Mauritania.