Uchaguzi wa Bunge Senegal unafanyika kesho Jumapili huku mivutano ya kisiasa ikiongezeka
Wananchi wa Senegal waliotimiza masharti ya kupiga kura kesho wataelekea katika masanduku ya kupigia kura kwa ajili ya kuwachagua wawakilishi wao wa Bunge.
Tume ya Uchaguzi ya Senegal imetangaza kuwa, maandalizi yote kwa ajili ya uchaguzi huo wa Bunge yamekamilika na kwamba, vifaa vyote vya kupigia kura vimeshapelekwa katika vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo kuna taarifa kwamba, kati ya wapiga kura milioni sita na laki mbili waliotimisha masharti ya kupigia kura, kuna wapiga kura wapatao laki saba ambao bado hawajapata vitambulisho vyao vya kura kukiwa kumebakia masaa machache kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo wa Bunge unafanyika kesho nchini Senegal katika hali ambayo, mvutano kati ya serikali ya nchi hiyo na vyama vya upinzani unaripotiwa kuongezeka mno katika siku za hivi karibuni.
Meya wa jiji la Dakar Khalifa Sall ambaye anawania kiti cha ubunge katika uchaguzi wa kesho angali anashikiliwa kifungoni.
Wapinzani nchini Senegal wanaituhumu seikali ya Rais Macky Sall kwamba, imekuwa ikikandamiza wapinzani.
Ripoti zinaonyesha kuwa, kuna wapinzani wengi waliotiwa mbaroni tangu Machi mwaka huu na ambao wangali wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya usalama akiwemo meya wa mji wa Dakar Khalifa Sall.
Senegal ilipata uhuru wake mwaka 1960 kutoka kwa mkoloni wa Ulaya, Ufaransa na kuanzia wakati huo hadi leo inatawaliwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia.