Chama cha upinzani Congo chatuhumiwa kushiriki katika mashambulizi ya Kinshasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32536-chama_cha_upinzani_congo_chatuhumiwa_kushiriki_katika_mashambulizi_ya_kinshasa
Msemaji wa Polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, idadi kadhaa ya wajumbe wa chama cha upinzani cha UPDS walikuwa katika kundi la watu waliofanya mashambulizi katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa.
(last modified 2026-04-28T05:09:17+00:00 )
Jul 31, 2017 22:08 UTC
  • Chama cha upinzani Congo chatuhumiwa kushiriki katika mashambulizi ya Kinshasa

Msemaji wa Polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, idadi kadhaa ya wajumbe wa chama cha upinzani cha UPDS walikuwa katika kundi la watu waliofanya mashambulizi katika mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa.

Pierrot Mwanamputu amesema kuwa, wanachama hao wa chama cha upinzani cha UPDS walioshiriki katika mashambulizi ya Kinshasa wametambuliwa, na kwamba Tshimanga Ben Tshimanga aliyepanga mashambulizi hayo alitumia waasi wa kundi la Kamwina Nsapu kutekeleza hujuma hiyo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi la Congo ameongeza kuwa, Tshimanga Ben Tshimanga ni afisa wa protokali wa chama kikuu cha upinzani cha UPDS. 

Hata hivyo Katibu Mkuu wa chama cha UPDS, Félix Tshisékedi amekadhibisha madai hayo na kutoa wito wa kuhukumiwa kiadilifu watuhumiwa wa mashambulizi hayo ili kuweka wazi uhakika wa mambo.  

Jela ya kangbaya, Beni

Mashambulizi yaliyofanyika tarehe 10 Juni mjini Kinshasa dhidi ya kituo cha polisi na ofisi ya mwendesha mashtaka yalipelekea kutoroka wafungwa 17 na kuua afisa mmoja wa polisi. Polisi wengine wanne walijeruhiwa vibaya. 

Mashambulizi hayo ya Kinshasa yalifuatiwa na yale yaliyolenga jela ya Kangwayi katika mji wa Beni tarehe 11 mwezi huo huo wa Juni ambapo watu 11 wakiwemo maafisa 8 wa polisi waliuawa na wafungwa 900 wakatoroka.