Ushindi wa chama tawala nchini Senegal katika uchaguzi wa Bunge
Chama tawala nchini Senegal kimejipatia ushindi katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika Jumapili iliyopita na hivyo kudhibiti wingi wa viti katika Bunge la nchi hiyo.
Mahammed Abdallah Dionne Waziri Mkuu wa Senegal sambamba na kutangaza ushindi wa muungano unaoungwa mkono Rais Macky Sall wa nchi hiyo amesema kuwa, muungano huo umefanikiwa kujikusanyia wingi wa ukura katika miji 45 ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Muungano unaoongozwa na Khalifa Sall Meya wa mji wa Dakar ambaye hadi sasa angali jela umeshika nafasi ya pili ukifuatiwa na muungano ulioundwa na Abdoulaye Wade Rais wa zamani wa Senegal.
Khalifa Sall meya wa Dakar ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa muungano wa Rais Macky Sall kwa miezi kadhaa sasa anashikiliwa kifungoni kwa tuhuma za ubadhirifu wa mali ya umma. Hata hivyo wapinzani nchini humo wanaitaja hatua hiyo kwamba, ilikuwa na malengo ya kisiasa.
Akthari ya makundi ya kisiasa yalilalamikia vikali hatua hiyo. Vyama 47 na miungano ya kisiasa vilichuana katika uchaguzi wa mara hii wa Bunge nchini Senegal, jambo ambalo liliongeza uwezekano wa kugawanyika kura na ushiriki mdogo wa wananchi katika uchaguzi huo.
Kuhusiana na suala hilo, gazeti la Le Monde la Ufaransa liliandika kabla ya kufanyika uchaguzi huo kwamba, kuweko vyama na miungano mingi ya kisiasa katika uchaguzi wa Senegal ambako hakukutarajiwa kutawachanganya wapiga kura.
Pamoja na hayo, ushiriki wa wapiga kura katika uchaguzi wa mara hii wa Bunge nchini Senegal unatajwa kuwa mkubwa ukilinganisha na uchaguzi wa hapo kabla.
Licha ya kuwa vyama vya upinzani vilijitahidi kuikosoa serikali ya Rais Macky Sall ili kuleta anga mpya na kuwashawishi wapiga kura wawachague wapinzani, lakini kuna mambo kadhaa yanayotajwa na weledi wa mambo kwamba, yaliwakwamisha wapinzani hao katika kufikia malengo yao.
Utendaji uliokuwa na mafanikio ya kiwango fulani wa Rais Macky Sall katika uga wa uchumi na wananchi kuridhika na sera zake na vile vile kuweko utitiri wa vyama vya upinzani na wakati huo huo kutokubaliana vyama hivyo kuunda muungano mmoja wenye nguvu ni baadhi ya mambo yanayotajwa na wajuzi wa mambo kwamba, yamechangia wapinzani hao kushindwa kufikia malengo yao.
Wapinzani hao walikuwa na matumaini kwamba, wangeweza kupata wingi wa viti vya Bunge na hivyo kupata nguvu ya kuishinikiza serikali ya Rais Macky Sall. Wapinzani nchini Senegal wamekuwa wakilalamikia kile wanachotaja kuwa, kutokuweko uhuru wa kisiasa na kukandamizwa wapinzani.
Fadel Barro, mratibu wa harakati ya kiraia nchini Senegal amelaani vikali kutiwa mbaroni na kufungwa jela wapinzani wengi na kusisitiza kama ninavyomnukuu: "Katu hatutakubali Senegali igeuzwe na kuwa uwanja wa mchezo."
Katika upande mwingine akthari ya waangalizi wa uchaguzi wa Senegal wameutathmini uchaguzi huo kama kura ya maoni ya serikali kupima utendaji wake na kiwango cha ridhaa ya wananchi kwa utendaji wa Rais Sall.
Wanasema kuwa, ushindi wa chama tawala katika uchaguzi wa Bunge, umemuandalia mazingira Rais Macky Sall ya kutetea vyema kiti chake cha Urais katika uchaguzi ujao uliopangwa kufanyika mwaka 2019.
Pamoja na hayo inaonekana kuwa, Rais Macky Sall anakabiliwa na kibarua kigumu katika kipindi hiki cha miaka miwili iliyobakia ya duru yake ya kwanza ya uongozi, hasa baada ya kurejea nchini humo Rais wa zamani wa nchi hiyo Abdoulaye Wade