Hali ya wasiwasi yashtadi katika kukaribia uchaguzi mkuu Kenya
Hali ya wasiwasi imeongezeka huko Kenya ikiwa zimesalia siku chache hadi kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo tarehe 8 Agosti.
Shirika la Habari la France 24 limeripoti kuwa uchaguzi mkuu wa Kenya utafanyika siku sita zijazo, hata hivyo kuuliwa siku kadhaa zilizopita mmoja wa maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo (IEBC) kumezitia wasiwasi taasisi za kiraia na waangalizi wa kimataifa. Chris Msando aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) juzi Jumatatu alipatikana akiwa ameaga dunia siku tatu baada ya kutoweka. Kitengo cha Tehama cha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya kimesema kuwa kuwa afisa hiyo aliteswa kabla ya kuuawa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kufuatia kuuawa afisa huyo wa uchaguzi wa Kenya, jana Jumanne makumi ya wanaharakati wa taasisi za kiraia za nchi hiyo waliandamana katika mitaa ya mji mkuu Nairobi kulaani mauaji hayo.
Hii ni katika hali ambayo waathirika wa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini Kenya pia wamekumbwa na wasiwasi wakihofia kutokea machafuko mengine nchini humo. Ghasia na machafuko yaliyoikumba Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 yalisababisha vifo vya watu 1100 na kuwafanya mamia ya raia wengine wa nchi hiyo kuikimbia nchi. Wananchi wa Kenya tarehe 8 mwezi huu wataelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kumchagua Rais wao mpya, wabunge na magavana.