Wapinzani waandamana Guinea Conakry juu ya uchaguzi, usalama
Maelfu ya wafuasi wa kambi ya upinzani huko Guinea Conakry wamefanya maandamano katika mji mkuu Conakry kulalamikia ucheleweshwaji wa uchaguzi sambamba na kuzidi kuwa mbaya hali ya usalama nchini humo.
Katika maandamano hayo ya jana Jumatano, waandamanaji walisikika wakidai kuwa serikali ya Rais Alpha Conde wa nchi hiyo inapanga njama ya kufanyia mabadiliko katiba ili kiongozi huyo aendelee kung'ang'ania madaraka.
Cellou Dalein Diallo, kinara wa upinzani nchini humo amewaambia waandishi wa habari katika eneo la Cosa, ambalo ni moja ya ngome za upinzani kuwa, wananchi wameamua kufanya maandamano kushinikiza kuheshimiwa sheria, kuimarishwa usalama na kulindwa haki.
Oktoba mwaka jana, Conde na Diallo walisaini makubaliano ya kuandaliwa uchaguzi wa Umeya kufikia mwezi Februari mwaka huu, lakini hadi sasa haujafanyika, kutokana na kile vyombo vya usalama vinasema ni kushtadi kwa hali ya taharuki na mizozo ya kisiasa.
Wapinzani wanamtuhumu Rais Conde kuwa anapanga kuifanyia mabadiliko katiba, ili aruhusiwe kugombea urais kwa muhula wa tatu mwaka 2020.
Huku maandamano na malalamiko ya wapinzani yakiendelea kufanyika nchini humo, duru za upinzani zinasema kuwa makumi ya waandamanaji waliuawa katika maandamano ya upinzani yaliyofanyika nchini humo miaka minne iliyopita.