Rais Kagame ahifadhi kiti chake katika uchaguzi wa Rwanda
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais nchini Rwanda yameonyesha kuwa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo amehifadhi kiti chake baada ya kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo uliofanyika jana Ijumaa.
Katibu Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Rwanda, Charles Munyaneza amewaambia waandishi wa habari mjini Kigali kuwa, Rais Kagame amepata asilimia 98.6 kwenye asilimia 80 ya matokeo yaliyokwisha hesabiwa hadi sasa. Baadhi ya duru za habari zinasema Kagame ameshinda kwa asilimia 99 katika asilimia 98 ya matokeo kwenye majimbo yote ya nchi.
Munyaneza amesema kwa mujibu wa mahesabu ya tume hiyo , hakuna kikubwa kinachotarajiwa kubadilika baada ya kuhesabiwa matokeo yote ya kura za urais. Tume ya uchaguzi Rwanda kadhalika imesema kuwa rais Kagame amezoa asilimia 98.95 ya kura za Wanyarwanda waishio nje ya nchi.
Kagame ambaye alishinda muhula wa pili kwa asilimia 93 katika uchaguzi wa mwaka 2010, hapo jana baada ya kupiga kura yake katika kituo cha Rugunga mjini Kigali aliwaambia wanahabari kuwa, ana uhakika wa kuibuka mshindi kutokana na rekodi yake ya maendeleo na kwamba uchaguzi huo ni urasimu tu.
Matokeo hayo ya awali kadhalika yanaonyesha kuwa mgombea huru wa kiti hicho Philippe Mpayimana amepata asilimia 0.72 huku Frank Habineza, mgombea wa chama cha Democratic Green Party of Rwanda akipata asilimia 0.45.
Rais Kagame ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2000, amekuwa akisifiwa na duru mbalimbali kutokana na jitihada zake za kurejesha amani nchini humo baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994, ambapo Watutsi laki 800 na Wahutu wenye misimamo ya wastani waliuawa.
Hata hivyo wakosoaji wake wamekuwa wakimkosoa vikali kwa kukandamiza upinzani na wanaoikosoa serikali, sanjari na kuzuia uhuru wa kujieleza.