AU: Wakenya wanataka uchaguzi huru, wa haki na wenye uwazi
Rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye anaongoza timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika AU nchini Kenya amesema wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki wanataka kuona zoezi hilo la Jumanne ijayo linafanyika katika mazingira huru, yenye haki na uwazi.
Katika kikao na waandishi wa habari mjini Nairobi jana Ijumaa, Thabo Mbeki amesema kama tunavyomnukuu: "Wakenya ambao tumeongea nao wametukaribisha kwa moyo mkunjufu na wanasema ni vyema tuchunguze uhalisia wa uchaguzi. Wanasema wanataka uchaguzi huru, wa haki na wenye uwazi."
Mbeki amesema jukumu la timu hiyo ya AU yenye waangalizi 103 ni kuchunguza, kutathmini, kudadisi na kuandika ripoti ya shughuli hiyo ya uchaguzi na kusisitiza kuwa, waangalizi hao hawataandika ripoti nzuri iwapo matukio yataenda kinyume na inavyotarajiwa na kinyume chake.
Mbali na Thabo Mbeki, shakhsia wengine walioko kwenye timu za waangalizi elfu tano wa ndani na nje ya nchi ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Marekani John Kerry, Rais Mstaafu wa Ghana John Dramani Mahama na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Patricia Scotland, miongoni mwa wengine.
Wananchi wa Kenya Jumanne ijayo ya tarehe 8 mwezi huu wataelekea kwenye masanduku ya kupigia kura kuchagua rais wao mpya, wabunge, magavana na wawakilishi wa wadi.
Katika uchaguzi wa rais, mchuano mkali unatarajiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee anayewania muhula wa pili, na kinara wa muungano wa NASA Raila Odinga, anayegombea kiti hicho kwa mara ya nne sasa.