Wanyarwanda wamkabidhi tena Paul Kagame usukani wa kuongoza nchi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32730-wanyarwanda_wamkabidhi_tena_paul_kagame_usukani_wa_kuongoza_nchi_yao
Paul Kagame, Rais wa sasa wa Rwanda amechaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka saba baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika jana kote nchini humo.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 05, 2017 08:32 UTC
  • Wanyarwanda wamkabidhi tena Paul Kagame usukani wa kuongoza nchi yao

Paul Kagame, Rais wa sasa wa Rwanda amechaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka saba baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika jana kote nchini humo.

Matokeo aliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi yanaonesha kuwa, Kagame amewapiku wapinzani wake wawili kwa kupata zaidi ya asilimia 98 ya kura zilizopigwa. Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda imesema, asilimia 97 ya Wanyarwanda waliotimiza masharti wameshiriki katika zoezi hilo.

Wapinzani wa Paul Kagame katika uchaguzi wa jana walikuwa Philippe Mpayimana wa kujitegemea na Frank Habineza, aliyebeba bendera ya Democratic Green Party of Rwanda ambao wamepata asilimia 0.72 na 0.45 kwa mpangilio.

Baada ya kupiga kura hiyo jana, Frank Habineza alikosoa tena sera za rais mteule, Paul Kagame akisema chama tawala cha RPF-Inkotanyi kimetumia suhula na vyombo vyote vya dola. Amesema kampeni zake za uchaguzi zilivurugwa na kutatizwa na kwamba hakuwa na uwezo wa kukabiliana na kampeni za mgombea wa chama tawala. Katika kampeni zake za uchaguzi pia Frank Habineza aliahidi kuwa, iwapo angeshinda uchaguzi wa jana angeunda mahakama ya kushughulikia tena kesi za wapinzani waliohukumiwa vifungo jela kwa sababu za kisiasa. 

Image Caption

Kagame ambaye ameshinda kiti cha Rais wa Rwanda kwa mara ya tatu mfululizo, aliingia Kigali mwaka 1994 na jeshi la wapiganaji wa RPF na kukomesha mauji ya kimbari yaliyofanywa na Wahutu wenye misimamo mikali dhidi ya Watutsi. Katika chaguzi za rais za mwaka 2003 na 2010, Paul Kagame alipata zaidi ya asilimia 90 ya kura za wananchi. Mwaka 2015 kiongozi huyo aliitisha kura ya maoni ya kuifanyia marekebisho katiba ya Rwanda na kuondoa kipengee cha mihula miwili tu ya rais, suala ambalo lilimpa tena fursa ya kugombea kiti hicho kwa mara ya tatu. Uamuzi huo ulikosolewa na wapinzani wake ndani ya nchi na hata katika duru za kimataifa.

Katika kipindi cha utwala wake, Kagame amefanikiwa kuhuisha uchumi uliokuwa umeporomoka wa nchi hiyo na kuzidisha kasi ya ustawi wa Rwanda kwa kutumia njia ya huduma na teknolojia ya mpya na kuboresha kilimo. Kwa kutilia maanani suala hilo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, ushindi wa kisiasa wa Paul Kagame ni matunda ya utendaji wake mzuri katika medani ya uchumi. Hata hivyo wachambuzi wengine wa mambo wanamkosoa sana kiongozi huyo wakisema, licha ya maendeleo hayo ya kichumi na kurejesha nidhamu ndani ya nchi hiyo baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, lakini amekuwa na rekodi mbaya katika baadhi ya mambo kama vile kuzima sauti ya wapinzani na vyombo vya habari vya kujitegemea na kuwakandamiza wapinzani wake wa kisiasa. Wachambuzi hao wanatia nguvu madai hayo kwa kusema: Katika kipindi cha miaka kadhaa ya utawala wake, idadi kubwa ya wapinzani wameuawa, kufungwa jela au kulazimika kwenda uhamishoni.

Mkuu wa zamani wa jeshi la Rwanda, Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa aliyekimbia nchi baada ya kuhitilafia na Kagame 

Vilevile shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kuhusu mauaji yanayofanyia kinyume cha sheria nchini Rwanda kwamba, wimbi la mauaji hayo linashuhudiwa nchini humo na kwamba inaonekana kuwa ni sehemu ya mbinu rasmi ya kueneza hofu na woga na kuzuia aina yoyote ya upinzani dhidi ya siasa za serikali.

Kwa vyoyote vile, inapasa kusema kuwa, kipindi cha utawala wa Paul Kagame nchini Rwanda kimeshuhudia ustawi na maendeleo ya kiuchumi na nidhamu ndani ya nchi hiyo ndogo ambayo miaka kadhaa iliyopita ilikaribia kusambaratika kabisa kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Hata hivyo rais mteule, Paul Kagame anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuboresha zaidi faili lake la kisiasa na masuala ya haki za binadamu, na kuwapa wapinzani wake uwanja mkubwa zaidi wa kujieleza na kukosoa utendaji wake.