Wapinzani nchini Kongo DR waitisha mgomo wa nchi nzima dhidi ya serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32872-wapinzani_nchini_kongo_dr_waitisha_mgomo_wa_nchi_nzima_dhidi_ya_serikali
Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameitisha mgomo wa nchi nzima dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 08, 2017 10:19 UTC

Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameitisha mgomo wa nchi nzima dhidi ya serikali ya Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo.

Watu 14 waliuawa kwa kupigwa risasi katika vurugu zilizotokea Jumatatu ya jana katika jiji la Kinshasa na mji wa Matadi, kusini mwa nchi hiyo. Kufuatia hali hiyo wapinzani wa serikali wameitisha mgomo wa nchi nzima leo na kesho kupinga mwenendo huo wa serikali sambamba na kuishinikiza serikali kutangaza tarehe ya uchaguzi. Polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa, vinara wa kundi la Bundu dia Kongo ndio waliohusika na vurugu hizo za jana. Hii ni katika hali ambayo kiongozi wa kundi hilo bado yupo mafichoni tangu alipotoroka jela za nchi hiyo tangu mwezi Mei mwaka huu.

Wafuasi wa kundi la Bundu dia Kongo

Inaelezwa kuwa ghasia hizo zilitokea baada ya shambulio kufanywa na wanachama wa kundi hilo la BDK katika jela kuu ya Kinshasa na maandamano yaliyofanywa na wanachama wengine wa kundi hilo dhidi ya Rais Joseph Kabila huko katika mji wa Matadi na katika mji wa Boma kusini magharibi mwa Kongo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikumbwa na mgogoro tangu serikali ya nchi hiyo ilipoahirisha uchaguzi na hatua ya Rais Joseph Kabila kuendelea kusalia madarakani. Licha ya kutiwa saini makubaliano kati ya serikali na wapinzani hapo tarehe 31 Disemba mwaka jana, ambayo yaliainisha tarehe ya kufanyika uchaguzi huo, lakini weledi wa mambo wanabaidisha kufanyika uchaguzi huo katika tarehe hiyo.