Mtawa wa India aokoa wanawake wa Kiafrika kutoka kwenye utumwa wa ngono
(last modified Thu, 10 Aug 2017 07:07:36 GMT )
Aug 10, 2017 07:07 UTC
  • Mtawa wa India aokoa wanawake wa Kiafrika kutoka kwenye utumwa wa ngono

Mtawa wa India aliyeokoa wanawake wa Cameroon kutoka kwenye utumwa wa ngono katika eneo la Mashariki ya Kati ametoa wito wa kutolewa misaada kwa wahanga hao ili kusaidia mchakato wa kuwarejesha kwenye hali ya kawaida na kuwaondoa kwenye mfadhaiko wa kinafsi uliosababishwa na manyanyaso ya aina mbalimbali kama ya kubakwa, kunajisiwa na kushikiliwa mateka.

Vanaja Jasphine anasema, ametambua wanawake zaidi ya 200 ambao wamechukuliwa kutoka nchi hiyo ya katikati mwa Afrika na kufanywa watumwa katika eneo la Mashariki ya Kati katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka jana mtawala huyo pia alisaidia jitihada za kuwarejesha nchini Cameroon wahanga 14 wa magenge ya magendo ya binadamu.

Ripoti zinasema kuwa, idadi kubwa ya wanawake wa Kiafrika wamekuwa wakipelekwa katika nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati kwa ajili ya kutafuta ajira na kazi za majumbani na maara nyingi hutumbukizwa katika utumwa mamboleo baada ya kunyang'anywa pasi zao za kusafiria.

Mtawa Vanaja Jasphine

Baadhi ya wanawake hao hufanywa watumwa wa ngono na kubakwa kila siku na pengine kulazimishwa kufanya ngono na wanyama.

Vanaja Jasphine anasema wanawake hao wanarejeshwa nchini wakiwa katika hali ya mfadhaiko na matatizo mengi ya kinafsi na ametoa wito wa kusaidiwa. Vilevile amezitaka serikali za Kiafrika kutoa misaada zaidi kwa wanawake wanaorejea nchini baada ya kuokolewa kwenye  utumwa wa ngono nje ya nchi.