EU yazitaka pande zote kuheshimu sheria nchini Kenya
Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa unafuatilia kwa makini mwenendo wa uchaguzi wa hivi karibuni huko Kenya.
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa kuwa umoja huo sawa kabisa na Umoja wa Afrika unataraji kwamba pande husika huko Kenya zitatekeleza majukumu yao ipasavyo kama ilivyobainishwa na katiba ya nchi hiyo.
Bi Federica Mogherini ameongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unatumai kwamba maafisa husika nchini Kenya watafatilia kwa makini malalalamiko yote yaliyowasilishwa kuhusu madai ya kufanyika udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa Jumanne iliyopita na kuchunguza kikamilifu iwapo kura zimeibiwa.
Baadhi ya wananchi wa Kenya wamefanya maandamano nchini humo na kusababisha ghasia na mapigano na askari usalama kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na kiongozi wa muungano wa upinzani NASA, Raila Odinga ambaye pia ni mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya muungano huo kwamba kumefanyika udanganyifu katika uchaguzi wa Kenya. Watu kadhaa wameuawa katika ghasia hizo.
Wakati huo waangalizi wa kimataifa wamewatolea wito Wakenya na upande wa upinzani kudumisha amani na utulivu na kusisitiza kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nch hiyo (IEBC) iendelea na shughuli zake. Matokeo ya awali ya uchaguzu wa Rais wa Kenya uliofanyika Agosti 8 yanaonyesha kuwa Rais Uhuru Kenyatta ameshinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 55 ya kura.