Mwili wa Tshisekedi kusafirishwa Kongo DR hivi karibuni
Mwili wa Mzee Étienne Tshisekedi, aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa chama cha The Union for Democracy and Social Progress UPDS huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unatazamiwa kusafirishwa nchini mwezi ujao kutoka Ubelgiji alikofia mwezi Februari mwaka huu.
Familia ya Tshisekedi na wakuu wa chama cha UPDS wameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mwili wa mwanasiasa huyo mkongwe utarejeshwa Kongo DR mwanzoni mwa mwezi ujao wa Septemba, na unatazamiwa kuzikwa nyumbani kwake katika mji wa N'sele, yapata kilomita 80 kutoka mji mkuu Kinshasa.
Upinzani nchini humo umekuwa ukisisitiza kuwa, mwili wa kiongozi wao huyo, unafaa upewe heshima ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kuzikwa katika majengo ya Bunge.
Wamesema baada ya vuta nikuvute, serikali imekubali kugharamia usafiri wa mwili na maziko ya kitaifa ya mwanasiasa huyo wa DRC.
Wadadisi wa mambo wanasema Tshisekedi alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe na shupavu na ambao walikuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia katika nchi hiyo ya Kiafrika, na kufa kwake kuliacha pengo kubwa katika medani ya kisiasa sio tu katika nchi hiyo, bali pia kieneo.
Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka jana 2016, Tshisekedi alirejea Kinshasa kutoka Ubelgiji alikokwenda kwa ajili ya matibabu miaka miwili nyuma. Maelfu ya wafuasi wake walifurika katika uwanja wa ndege na vilevile kujipanga katika barabara ya kuelekea kwao Limete kumlaki kiongozi huyo mkongwe wa upinzani ambaye kurejea kwake nchini kulitazamiwa kupiga jeki harakati za wapinzani.