Aug 15, 2017 16:17 UTC
  • Walinganiaji wa Qur'ani kutoka Kuwait wauawa katika shambulizi la Burkina Faso

Walinganiaji wawili wa Qur'ani kutoka Kuwait ni miongoni mwa raia wa kigeni waliouawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga mgahawa wa Aziz Istanbul katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou usiku wa kuamkia jana.

Katika shambulizi hilo lililofanywa na watu wasiojulikana, watu 18 wakiwemo raia 8 wa nchi za kigeni waliuawa na wengine 8 kujeruhiwa. 

Dr Walid Al Ali, mhadhiri wa kitivo cha sheria katika Chuo Kikuu cha Kuwait ambaye pia ni mhubiri wa Msikiti Mkuu wa nchi hiyo na Sheikh Fahd Al Hussaini aliyekuwa mwalimu wa Qur'ani waliaga dunia katika shambulizi hilo baada ya watu hao waliokuwa na silaha kuvamia mgahawa huo maarufu wa Waturuki na kufyatua risasi ovyo. 

Walinganiaji hao wawili walikuwa wakipata chakula cha usiku katika mgahawa huo wa Aziz Istanbul ulio karibu na Hoteli ya Bravia walipokuwa wamefikia.

Baadhi ya wahanga wa shambulizi la mgahawa wa Aziz Istanbul

Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Alpha Barry amesema raia wengine wa nchi za kigeni waliouawa katika shambulizi hilo ni kutoka nchi za Canada, Ufaransa, Lebanon, Nigeria, Senegal na Uturuki.

Mgahawa wa Aziz Istanbul uko umbali wa mita 100 tu kutoka Hoteli ya Cappuccino Café iliyoshambuliwa na magaidi Januari mwaka jana wa 2016 ambapo watu 30 waliuawa wengi wao wakiwa raia wa nchi za kigeni. 

Tags