Ghannouchi na wanaharakati wa kisiasa wagoma kula kuonyesha mshikamano na Ben Mbarek
-
Rached Ghannouchi
Timu ya utetezi ya Rached Ghannouchi, spika wa zamani wa Bunge la Tunisia na mkuu wa harakati ya Ennahda, ilitangaza jana Ijumaa kwamba mwanasiasa huyo mkongwe ameanza mgomo wa kula usio na kikomo kuonyesha mshikamano na Jaouhar Ben Mbarek, ambaye ni miongoni mwa viongozi wa kundi la National Salvation Front and Citizens Against the Coup linalompinga Rais wa Tunisia, Kais Saied.
Ben Mbarek ambaye amekuwa kizuizini katika gereza la Belli katika jimbo la Nabeul tangu Oktoba 29, alianza mgomo wa kula bila kikomo kupinga kukamatwa kwake kwa madai ya kula "njama dhidi ya usalama wa taifa".
Taarifa iliyotolewa na timu ya utetezi ya Ghannouchi kwenye Facebook imesema, Ghannouchi ameanza mgomo wa kula usio na kikomo kuonyesha mshikamano wake na Ben Mbarek na kutetea kujitegemea kwa mahakama na uhuru nchini.
Mwezi Aprili mwaka huu, mahakama ya Tunisia ilimhukumu Ben Mbarek, profesa wa sheria ya katiba katika Chuo Kikuu cha Tunis, kifungo cha miaka 18 jela katika kesi ya kula "njama dhidi ya usalama wa taifa".
Makundi ya upinzani, ikiwa ni pamoja na National Salvation Front, yanasema kesi hiyo ni "ya kisiasa na inatumika kuwafutilia mbali wapinzani wa kisiasa" wa Rais Kais Saied.
Mapema Ijumaa, wanaharakati wa kisiasa nchini Tunisia walitangaza kwamba wameanza mgomo wa kula kuonyesha mshikamano wao na Jaouhar Ben Mbarek. Tangazo hilo limetolewa kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na "Uratibu wa Familia za Wafungwa wa Kisiasa nchini Tunisia" katika makao makuu ya Chama cha Republican cha Tunisia mjini Tunis.
Takriban washtakiwa 40, akiwemo Ben Mbarek, walifikishwa mahakamani kwa pamoja mwezi Machi, wakikabiliwa na mashtaka ya "kupanga njama dhidi ya usalama wa taifa" na "kushirikiana na kundi la kigaidi".
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaani kesi hiyo ya halaiki likiitaja kuwa ni "kejeli" na kuihimiza Tunisia "kuwaachilia huru mara moja" wote walioshtakiwa.