Idadi ya waliopoteza maisha katika maporomoko ya udongo DRC imepindukia 200
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33332-idadi_ya_waliopoteza_maisha_katika_maporomoko_ya_udongo_drc_imepindukia_200
Idadi ya watu waliopoteza maisha katika janga la kimaumbile la maporomoko ya udongo katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongezeka na kupindukia watu 200.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 19, 2017 02:31 UTC
  • Idadi ya waliopoteza maisha katika maporomoko ya udongo DRC imepindukia 200

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika janga la kimaumbile la maporomoko ya udongo katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongezeka na kupindukia watu 200.

Pacifique Keta, Naibu Gavana wa mkoa wa Ituri amewaambia waandishi wa habari kwamba, zaidi ya watu mia mbili wamepoteza maisha katika tukio la maporomoko ya udongo lililotokea siku ya Alkhamisi katika kijiji cha uvuvi cha Tora katika ukanda wa Ziwa Albert kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Naibu Gavana huyo wa mkoa wa Ituri ameongeza kuwa, watu wengi walifukiwa na udongo katika tukio hilo na kwamba, juhudi za uokozi zinaendelea licha ya kukabiliwa na mazingira magumu kutokana na uchache wa suhula.

Mkoa wa Ituri mahali palipotokea maporomoko ya udongo

Janga hilo la kimaumbile la maporomoko ya udongo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetanguliwa na maafa mengine kama hayo nchini Sierra Leono ambapo zaidi ya watu mia nne wanaripotiwa kupoteza maisha huku mia 600 wakiwa bado hawajulikani waliko.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikikumbwa mara kwa mara na matukio ya aina hiyo pamoja na mafuriko ambapo mwezi Mei mwaka 2010 maporomoko ya udongo yalikumba kijiji cha Kibiriga mashariki mwa nchi hiyo na kuua watu 19. Kadhalika mwezi Februari mwaka 2002, watu 50 walipatikana wakiwa wamekufa baada ya wimbi la tope na majabali kuukumba mji wa mashariki wa Uvira na kudidimiza nyumba zipatazo 150.