Ahmad Bilal: Serikali ya Sudan inapinga kuwa na uhusiano na Israel
Waziri wa Habari wa Sudan ametangaza kuwa, serikali ya Khartoum inapinga kuanzishwa uhusiano baina yake na utawala wa Kizayuini wa Israel.
Ahmad Bilal ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa Sudan amesema hayo kufuatia matamshi yaliyozusha makelele mengi yaliyotolewa na Mubarak Fadel al-Mahdi Waziri wa Uwekezaji wa nchi hiyo ambaye alisema kuwa, hakuna kizuizi cha kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Sudan na Israel.
Akijibu matamshi hayo, Waziri wa Habari wa Sudan amesisitiza kuwa, serikali ya Khartoum haina azma wala mpango wa kuwa na uhusiano na utawala ghasibu wa Israel. Ahmad Bilal ambainisha kwamba, matamshi ya Mubarak Fadel al-Mahdi, Waziri wa Uwezekaji wa nchi hiyo, ni msimamo wake binafsi na sio msimamo wa serikali ya Khartoum.
Waziri huyo wa habari amesisitiza kwamba, msimamo rasmi wa serikali ya Sudan ni kwamba, nchi hiyo haina mpango wa kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Aidha katika sehemu nyingine ya matamshi yake hayo, Waziri wa Uwekezaji wa Sudan alisema kwamba, hakuna tatizo kwa Wapalestina kuanzisha uhusiano na Israel au hata Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kukaa na kufanya mazungumzo na Israel.
Waziri Mubarak Fadel al-Mahdi ametoa matamshi hayo, katika hali ambayo, serikali ya Sudan haiitambui rasmi Israel na wala haina uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu ambao umekuwa ukitenda jinai na mauaji kila siku dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.