Serikali ya DRC yawaita wapinzani katika meza ya mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33913-serikali_ya_drc_yawaita_wapinzani_katika_meza_ya_mazungumzo
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewaita wapinzani wa nchi hiyo katika meza ya mazungumzo ili kujaribu kutatua hitilafu zilizoko kati ya pande mbili hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2017 23:50 UTC
  • Serikali ya DRC yawaita wapinzani katika meza ya mazungumzo

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewaita wapinzani wa nchi hiyo katika meza ya mazungumzo ili kujaribu kutatua hitilafu zilizoko kati ya pande mbili hizo.

Wito huo wa mazungumzo umetolewa na Joseph Kapika Waziri wa Uchumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye amewataka waandaaji wa maaandamano yaliyopigwa marufuku na Meya wa jiji la Kinshasa kuitikia wito wa serikali wa kuweko mazungumzo baina ya pande mbili.

Waziri huyo wa serikali ya Rais Joseph Kabila amesisitiza kuwa, serikali  ya Kinshasa iko tayari kufanya mazungumzo na vyama vyote vya nchi hiyo na kwamba, matatizo na hitilafu zote zilizopo zinaweza kupatiwa ufumbuzi katika mazungumzo.

Kadhalika Waziri wa Uchumi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ameashiria maandamano ya utumiaji mabavu ambayo hutokea mara kwa mara nchini humo na kubainisha kwamba, malengo ya baadhi ya waandamanaji ni kuzusha machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu.

Rais Joseph Kabila anatuhumiwa na wapinzani kwamba anafanya njama za kuendelea kubakia madarakani licha ya kipindi chake cha uongozi kumalizika

Aidha Waziri Joseph Kapika amewataka wapinzani waachane na mpango wao wa maandamano waliyoyaitisha leo Jumatatu Septemba 4 akisisitiza kwamba, njia bora ya kutatua hitilafu ni kupitia mazungumzo.

Mgogoro wa ndani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo uliibuka baada ya kuahirishwa tarehe ya uchaguzi wa rais na kadhalika sisitizo la Rais Joseph Kabila la kutaka kuendelea kusalia madarakani nchini humo. Licha ya kutiwa saini makubaliano baina ya wapinzani na serikali juu ya kufanyika uchaguzi wa rais tarehe 31 mwezi Disemba mwaka huu, hata hivyo inaonekana kuwa, uchaguzi huo hautaweza kufanyika katika tarehe iliyopangwa.