Wafungwa karibu mia moja watoroka jela Ivory Coast
Wafungwa wapatao mia moja wameripotiwa kutoroka jela nchini Ivory Coast.
Vyombo vya mahakama vya Ivory Coast vimetangaza kuwa, wafungwa waliotoroka jela ya mji wa Katiola ni wafuasi wa kiongozi la waasi wa jela hiyo aliyeuawa mwaka jana, Coulibaly Yacouba.
Yacouba anayejulikana kama "Yacou Mchina" aliuawa Februari mwaka jana wa 2016 wakati wa jaribio la kutoroka jela kuu ya Abidjan nchini Ivory Coast. Watu 10 waliuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika jaribio hilo.
Maafisa usalama wa Ivory Coast wamesema kuwa, wafungwa 96 wametoroka mapema leo asubuhi kupitia paa za seli zao.
Hilo ni tukio la hivi karibuni zaidi la wafungwa kutoroka jela huko Ivory Coast nchi ambayo imekuwa ikisumbuliwa na machafuko na mivutano ndani ya jeshi la taifa.
Mwezi uliopita pia wafungwa watano walitoroka jela ya mji wa Gagnoa na vyombo vya usalama vinawashikilia walinzi wa gereza hilo kwa tuhuma za kula njama na wafungwa hao.