Wakimbizi wa Kongo DR waendelea kukimbilia nchini Zambia
Umoja wa Mataifa umetangaza ongezeko la wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini Zambia.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza Jumamosi ya leo kwamba tangu tarehe 30 Agosti hadi tarehe 6 ya mwezi huu wa Septemba yaani kipindi cha wiki moja, zaidi ya wakimbizi 1800 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokea maeneo ya mpakani ya nchi hiyo, wamewasili nchini Zambia.
Kwa mujibu wa shirika hilo, idadi ya wakimbizi wa Kongo DR walioingia Zambia kuanzia mwezi Januari mwaka huu hadi sasa imeongezeka na kufikia 4478, na hivyo kuifanya idadi kamili ya wakimbizi wa taifa hilo kubwa la katikati mwa Afrika walioko nchini Zambia kupindukia efu 25. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, kwa kuzingatia kuwa hadi sasa kungali kuna kundi la wakimbizi waliopiga kambi katika baadhi ya maeneo ya mpakani, kuna uwezekano wa wakimbizi zaidi wa Jamhuri ya Kiodemokrasia ya Kongo kuingia nchi hiyo jirani ya Zambia.
Machafuko yanayoambatana na mapigano kati ya jeshi la serikali na makundi ya wanamgambo katika maeneo ya Pweto na Muba yanatajwa kuwa sababu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika maeneo hayo kuyahama makazi yao.