Hizi hapa sababu za kuendelea mgogoro wa kisiasa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34171-hizi_hapa_sababu_za_kuendelea_mgogoro_wa_kisiasa_drc
Mtandao wa habari za redio na televisheni za Ubelgiji umesema kuwa, kufariki dunia Étienne Tshisekedi, mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kumezidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 10, 2017 10:07 UTC
  • Hizi hapa sababu za kuendelea mgogoro wa kisiasa DRC

Mtandao wa habari za redio na televisheni za Ubelgiji umesema kuwa, kufariki dunia Étienne Tshisekedi, mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa upinzani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kumezidisha mgogoro wa kisiasa nchini humo.

Mtandao huo wa habari za redio na televisheni za Ubelgiji (RTBF) umesema kuwa, kufariki dunia Tshisekedi ni pigo kubwa kwa wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hadi hivi sasa jambo hilo linasababisha kutokea matukio mengi ya kisiasa nchini humo.

Machafuko mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Mbali na vyama vya upinzani, mirengo ya kijamii na kidini nayo inapinga namna Rais Joseph Kabila anavyoendesha serikali na inataka mchakato wa makabidhiano ya madaraka ufanyike kwa usalama na amani.

Vyama vya upinzani vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo navyo vina uungaji mkono wa wananchi na vinamtaka Rais Joseph Kabila atekeleze ahadi zake za kuondoka madarakani na kuitisha uchaguzi katika muda uliopangwa.

Kuakhirishwa uchaguzi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kumezusha upinzani wa ndani ya nje ya nchi hiyo huku wapinzani wakisema kuwa, kuakhirishwa uchaguzi huo ni njama za Rais Joseph Kabila za kutaka kuendelea kubakia madarakani kwa muda mrefu zaidi.

Kipindi cha mwisho cha urais wa Joseph Kabila kilimalizika mwaka jana. Serikali ya Kinshasa inasema mazingira wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hayaruhusu kufanyika uchaguzi, suala ambalo limepingwa vikali na wapinzani.