Indhari ya WHO kuhusu mlipuko wa kipindupindu DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34187-indhari_ya_who_kuhusu_mlipuko_wa_kipindupindu_drc
Shirika la Afya Duniani WHO limetoa tahadhari juu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ambao hadi sasa umepelekea watu 528 kupoteza maisha na hivyo kufikia kiwango cha kutia hofu.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 10, 2017 22:49 UTC
  • Indhari ya WHO kuhusu mlipuko wa kipindupindu DRC

Shirika la Afya Duniani WHO limetoa tahadhari juu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ambao hadi sasa umepelekea watu 528 kupoteza maisha na hivyo kufikia kiwango cha kutia hofu.

Kwa mujibu wa WHO, ugonjwa wa kipindupindu umekuwa tatizo sugu DRC kwani kila mwaka mamilioni ya raia wakiugua nchini humo huambukizwa kipindupindu ambapo mwaka jana watu 817 walifariki dunia.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa aidha linasema mripuko wa kipindupindu nchini DRC umefikia hali mbaya ambapo majimbo 20 kati ya 26 yameathiriwa na ugonjwa huu.

Kulingana na takwimu za WHO kuna waathirika wa kipindupindu kati ya milioni moja nukta nne hadi milioni nne nukta tatu duniani kila mwaka na husababisha vifo takriban laki moja na elfu arobaini na mbili.

Watu wenye kipindupindu wakipata matibabu

Tarehe 2 September mamlaka za DRC zilirekodi kesi ishirini na nne elfu na mia mbili na kumi na saba za maambukizi ya kipindupindu.

Mripuko wa ugonjwa huo umeathiri miji kadhaa ya mashariki, magharibi, kaskazini na baadhi ya maeneo ya jiji la Kinshasa.

WHO imesema inatoa mchango wa dola laki nne kwa ajili ya wafanyakazi wa afya katika maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa huo huku serikali ya DRC ikitakiwa kuimarisha afya ya umma ili kuzuia kuenea kipindupindu.