Umoja wa Mataifa walaani jeshi la DRC kwa kuwaua wakimbizi kutoka Burundi
Umoja wa Mataifa umelaani vikali mauaji ya wakimbizi wasiopungua 36 kutoka Burundi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katika tukio la Ijumaa usiku, wakimbizi 36 wa Burundi waliuawa katika mapigano huko mjini Kamanyola mkoani Kivu Kusini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati wa maandamano ya kupinga kurejeshwa nyumbani kwa wenzao. Wakimbizi hao walipoteza maisha baada ya kupigwa risasi na wanajeshi wa DRC.
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaolinda amani nchini DRC MONUSCO, Maman Sidikou amethibitisha katika taarifa kuwa takribani wakimbizi 36 wameuawa na wengine 124 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa kuna wakimbizi 44 elfu wa Burundi walioko nchini DRC. Wakimbizi wa Burundi waliingia nchini humo baada ya kushtadi mzozo wa kisiasa nchini mwao mwaka 2015. Maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa kipindi cha miaka 20 sasa. Udhaifu wa jeshi la serikali na askari wa kofia ya buluu wa Umoja wa Mataifa, unatajwa kuwa chanzo cha ongezeko la machafuko maeneo hayo.