Rais wa Kenya: Hukumu ya Mahakama ya Juu ilikuwa ni "mapinduzi"
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34663-rais_wa_kenya_hukumu_ya_mahakama_ya_juu_ilikuwa_ni_mapinduzi
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ilifanya "mapinduzi" dhidi ya matakwa ya wananchi ilipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita ambao yeye alishinda.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 21, 2017 15:45 UTC
  • Rais wa Kenya: Hukumu ya Mahakama ya Juu ilikuwa ni

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ilifanya "mapinduzi" dhidi ya matakwa ya wananchi ilipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita ambao yeye alishinda.

Uhuru Kenyatta ameyasema hayo leo katika hotuba aliyotoa mubashara kupitia televisheni na kuongeza kuwa: "yamefanywa mapinduzi hivi karibuni nchini Kenya na watu wanne katika Mahakama ya Juu".

Rais wa Kenya amerudia tena msimamo wake wa kukosoa uamuzi wa mahakama hiyo kwa kusema: "Tumekipindua kila kitu ndani ya nchi hii kwa uamuzi wa watu wachache. Sijui historia itawahukumu vipi mabwana hawa. Raia ameambiwa kwamba hana sauti... Kama huu si udikteta, sijui basi niseme nini".

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya uliotangazwa tarehe Mosi ya mwezi huu wa Septemba ulikuwa wa kwanza kutolewa na chombo cha mahakama kubatilisha uchaguzi uliompa ushindi rais barani Afrika. Hatua hiyo ilitoa mtikisiko ndani na nje ya Kenya.

Mahakama ya Juu ya Kenya iliamuru uchaguzi wa marudio ufanyike ndani ya muda wa siku 60 kati ya Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye aliyapinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Agosti 8 na kuamua kufikisha malalamiko mahakamani. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) ilikuwa imemtangaza Rais Uhuru Kenyatta mshindi kwa wingi wa kura milioni moja na laki nne dhidi ya Odinga.

Jopo la majaji wa Mahakama ya Juu likitangaza uamuzi wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais

Japokuwa tume hiyo imetangaza Oktoba 17 kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio lakini kuna hatihati kama utaweza kufanyika kutokana na ripoti kwamba maandalizi yake bado hayajakamilika.

Jana Mahakama ya Juu ilitoa maelezo ya ufafanuzi kuhusiana na uamuzi wake wa kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti 8. 

Majaji watatu kati ya wanne waliopiga kura ya kubatilisha matokeo hayo wameilaumu IEBC kwa kuanza kupeperusha matokeo ya urais kabla ya kuyafanyia uhakiki wakisisitiza kuwa katiba, sheria na kanuni za uchaguzi zilikiukwa pakubwa.

Wamesisitiza kuwa, kasoro zilizokuwepo zilikuwa nyingi na zilizoratibiwa kwa makusudi kiasi cha kuathiri matokeo na kwamba suala la kutokuwepo uwazi katika upeperushaji wa matokeo pia linatia shaka.

Jana hiyo hiyo polisi nchini Kenya walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta ambao waliandamana nje ya Mahakama ya Juu wakipinga uamuzi wa kubatilisha uchaguzi huo wa rais.../