Kambi ya Upinzani Congo yapinga matamshi ya Kabila katika UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34815-kambi_ya_upinzani_congo_yapinga_matamshi_ya_kabila_katika_un
Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekosoa matamshi yaliyotolewa na Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Sep 25, 2017 03:19 UTC
  • Kambi ya Upinzani Congo yapinga matamshi ya Kabila katika UN

Wapinzani wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekosoa matamshi yaliyotolewa na Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Wapinzani wa serikali ya Congo wanasema madai yaliyotolewa na Rais Kabila kuhusu kile alichokiita matunda ya serikali yake ya kurejesha amani na utulivu wa kisiasa nchini humo hayana msingi.

Wamesema kuwa Kabila ndiye sababu kuu ya mgogoro wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wanaamini kwamba, hotuba iliyotolewa na kiongozi huyo katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa haikuwa na msingi kwa sababu Kabila amekataa kutayarisha mazingira mazuri ya kuitishwa uchaguzi huru na wa wazi. 

Joseph Kabila akihutubia Baraza Kuu la UN

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Rais Joseph Kabila wa Congo alisema kuwa, nchi hiyo inaelekea kwenye uchaguzi wa kuaminika, wa wazi na wa amani.

Matamshi hayo ya Kabila yametolewa baada ya wimbi kubwa la malalamiko ya ndani na nje ya nchi hiyo linalomlaumu kwa kuendelea kung'angania madaraka na baada ya taasisi za serikali ya Kinshasa kuashiria kwamba huenda uchaguzi wa rais usifanyike nchini huko mwishoni mwa mwaka huu kwa mujibu wa makubaliano ya serikali na kambi ya upinzani.