Polisi Kenya watawanya wapinzani wanaotaka mabadiliko tume ya uchaguzi
Polisi wa kuzima ghasia nchini Kenya wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakitaka baadhi ya maafisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC wafutwe kazi kabla ya uchaguzi wa rais wa marudio wa Oktoba 26.
Taarifa zinasema waandamanaji waliokuwa wamekusanyika nje ya makao makuu ya IEBC walitawanywa baada ya kuibua ghasia katika maandamano ambayo awali yalikuwa yametangazwa kuwa ni ya amani.
Mgombea urais wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga, ambaye alishindwa na hasimu wake wa jadi Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, atapata fursa ya kuwania kiti hicho baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo. Odinga, ambaye ameitisha maandamano ya leo, anasema hatoshiriki katika uchaguzi wa marudio iwapo baadhi ya maafisa wa uchaguzi anaodai kuwa walihusika na wizi wa kura hawatafutwa kazi na kushtakiwa.
Hii ni katika hali ambayo Mahakama ya Juu ambayo ilibatilisha matokeo ya uchaguzi haikumpata mtu yeyote na hatia lakini ilisema IEBC ilifeli kama taasisi kwa kukiuka taratibu na sheria katika utangazaji matokeo ya uchaguzi.
Wiki iliyopita Mwendesha Mashtaka Mkuu Kenya aliagiza maafisa 11 wa IEBC akiwemo mkurugenzi mtendaji, Ezra Chiloba ambaye Odinga anasisitiza afutwe kazi, wachunguzwe. Maandamano ya leo pia yameripotiwa katika miji ya Kisumu na Mombasa.
Jana Rais Uhuru Kenyatta alisema wapinzani wana haki ya kuandamana lakini akaonya kuwa serikali yake haitaruhusu waibue fujo na ghasia au kuharibu mali.