Sep 27, 2017 14:13 UTC
  • Waafrika Kusini waandamana kulaani ufisadi chini ya Rais Zuma

Maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano katika mji wa Cape Town kudhihirisha ghadhabu zao kutokana na kashfa mbalimbali za ufisadi, ukosefu wa ajira na kuzorota uchumi chini ya utawala wa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.

Waandamanaji hao wamekusanyika nje ya majengo ya Bunge mjini Cape Town, wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe zinazosema "Zuma aondoke", "Ufisadi ni jinai dhidi ya ubinadamu" na "Zuma lazima ajiuzulu".

Muungano Mkuu wa Vyama vya Wafanyakazi Afrika Kusini (COSATU) umewataka wanachama wake wapatao milioni moja kususia kazi na kujiunga na maandamano dhidi ya Zuma kote nchini.

Waandamanaji wakiwa na mabango mjini Cape Town

Ifahamike kuwa, COSATU ni muungano tanzu ndani ya chama tawala ANC kinachoongozwa na Rais Zuma.  

Mmoja wa waandamanaji hao kwa jina la Florence Titus ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: "Mambo yanaporomoka chini ya Zuma, ameshindwa kutekeleza jukumu lake kama rais na badala yake anajaza mifuko yake na ya familia yake."

Licha ya maandamano ya mara kwa mara na mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu, lakini Rais Zuma amekuwa akisisitiza kuwa atabakia madarakani hadi muhula wake wa kisheria utakapomalizika, mwaka 2019.

 

Tags