Wanaharakati 16 wa kisiasa waachiwa huru Congo DR
Maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametangaza kuwa, wamewaachia huru wanaharakati kadhaa wa kisiasa waliokuwa wametiwa nguvuni na vyombo vya usalama.
Ripoti zinasema kuwa, maafisa wa serikali ya Congo waliwaachia huru wanaharakati 16 wa kisiasa jana Jumapili maasa 12 baada ya kutiwa nguvuni na kuhojiwa na polisi.
Wanahakati hao walitiwa nguvuni Jumamosi iliyopita katika mji wa Kisangani wakati wa maandamano ya kutaka kufanyika uchaguzi wa rais nchini Congo hadi kufikia tarehe 31 Disemba mwaka huu.
Wanaharakati wengine 33 wa kisiasa walitiwa nguvuni Jumamosi iliyopita katika mji wa Goma makao makuu ya mkoa wa Kivu Kaskazini na hadi sasa wangali wanashikiliwa vya vyombo vya usalama.
Maandamano na harakati za kutaka kufanyika uchaguzi wa rais hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu zimekuwa zikishuhudiwa mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa Disemba 2016 kati ya Serikali ya Kinshasa na kambi ya upinzani, Rais Joseph Kabila aliahidi kukabidhi madaraka ya nchi mwishoni mwa mwaka huu na kuitisha uchaguzi huru na wa haki. Hata hivyo Tume ya Uchaguzi wa Congo imetangaza kuwa, yumkini uchaguzi huo usifanyike katika muda ulioainishwa.