Maelfu waandamana Ethiopia katika kumbukumbu ya mauaji ya Bishoftu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35141-maelfu_waandamana_ethiopia_katika_kumbukumbu_ya_mauaji_ya_bishoftu
Maelfu ya raia wa Ethiopia wameandamana katika kumbukumbu ya mauaji ya Bishoftu na kupiga nara kuilaani serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 02, 2017 14:28 UTC
  • Maelfu waandamana Ethiopia katika kumbukumbu ya mauaji ya Bishoftu

Maelfu ya raia wa Ethiopia wameandamana katika kumbukumbu ya mauaji ya Bishoftu na kupiga nara kuilaani serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn.

Maandamano hayo yaliyofanyika kwa mnasaba wa kukumbuka mauaji ya Bishoftu yamesisitiza juu ya udharura wa kuondolewa madarakani serikali ya chama tawala cha nchi hiyo.

Washiriki wa maandamano hayo wamelaani vikali mauaji ya mwaka jana katika mji wa Bishoftu ulioko kusini mashariki mwa mji mkuu Addis Ababa.

Ikumbukwe kuwa, mwaka jana makumi ya watu waliuawa katika mji wa Bishoftu  wakati walipokuwa wakiandamana kulalamikia mpango wa serikali wa kuupanua mji mkuu Addis Ababa. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Malalamiko na maandamano hayo dhidi ya serikali yalipelekea kutokea ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Licha ya serikali ya Ethiopia kutangaza kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha yao katika tukio hilo ilikuwa 55, lakini wapinzani wanasisitiza kwamba, takribani watu 150 waliuawa. Baada ya tukio hilo serikali ya Ethiopia ilitangaza hali ya hatari. 

Wakati huo huo, watu zaidi ya 50 wameuawa katika mapigano ya wiki moja katika maeneo ya Oromiya na Somali nchini Ethiopia huku wengine 50,000 wakilazimika kukimbia makazi yao. 

Wakazi wa maeneo hayo mawili wanarushiana lawama kuhusu chanzo cha kuibuka machafuko hayo. Mkuu wa mkoa wa Oromiya Lema Megersa amesema serikali itawachukulia hatua wahusika wa machafuko hayo.