Polisi ya Kenya yatumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa NASA
Polisi nchini Kenya wamelazimika kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa muungano wa upinzani NASA walioandamana katika miji ya Nairobi na Kisumu kushinikiza mabadiliko katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC.
Maandamano hayo yyaliyoitishwa na muungano wa upinzani wa NASA yanataka kuweko mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC ikiwa ni pamoja na kutimuliwa kwa baadhi ya maafisa wa tume hiyo.
Muungano wa upinzani nchini Kenya unasema unaongoza maandamano kushinikiza mabadiliko ndani ya tume hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio wa urais tarehe 26 mwezi huu wa Oktoba.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, wafuasi wa muungano wa NASA mapema leo walimiminika katika mitaa na barabara za mji mkuu Nairobi, Kisumu, Kakamega na Mombasa ambapo polisi walilazimika kuwatawanya kwa kutumia gesi ya kutoa machozi.
Mjini Kisumu maandamano hayo yalisababisha kukwaza huduma ya usafiri na kuleta matatizo mengi. Kiongozi wa muungano huo Raila Odinga ametangaza mara kadhaa kwamba, hawatakubali kufanyika uchaguzi huo iwapo madai yao hayatatekelezwa likiwemo suala la kutimuliwa baadhi ya maafisa wa uchaguzi.
Serikali ya Kenya imesema maandamano ya muungano wa upinzani yatadhibitiwa na vitengo vya kuimarisha usalama vya nchi hiyo. Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa ni haki ya wafuasi wa Nasa na viongozi wao kuandamana lakini ameonya kuwa serikali haitawaruhusu wasababishe fujo na matatizo kwa wengine wasiohusika na maandamano.
Uchaguzi wa marudio wa kiti cha urais umepangwa kufanyika tarehe 26 mwezi huu ambapo Raila Odinga mgombea wa muungano wa upinzani wa NASA atachuana tena na Rais Uhuru Kenyatta wa chama tawala cha Jubilee.