Mamia waandamana Morocco kutaka kuachiwa huru wanaharakati
Mamia ya wananchi wa Morocco wamefanya maandamano katika mji mkuu wa kibiashara wa nchi hiyo Casablanca, kushinikiza kuachiwa huru wanaharati wa nchi hiyo waliokamatwa katika maandamano mengine mwaka mmoja uliopita katika mji mmoja ulioko kaskazini mwa nchi, ambao wakazi wake wanadai kutengwa na kubaguliwa.
Katika maandamano hayo ya jana Jumapili, waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara zinazosema "Uhuru, Haki, Hadhi na Usawa wa Kijamii".
Nabila Mounib, Rais wa harakati ya Federation of the Democratic Left amewaambia waandishi wa habari katika maandamano hayo kuwa, "Tuko hapa kwa kuwa tumechoshwa, tumekuja kushinikiza kuachiwa huru wanaharati wenzetu na kutaka mazingira ya mazungumzo kuhusu matakwa yao yaandaliwe, na zaidi ya yote tumekuja kulaani ufisadi ambao umelitafuna eneo hili la Rif la kaskazini mwa nchi."
Katika maandamano ya hivi karibuni, maafisa usalama wa mji wa Al Hoceima walitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi katika jaribio la kuyawatawanya waandamanaji waliokuwa wakionyesha hasira zao kali kutokana na kutiwa nguvuni kiongozi wao, Nasser Zefzafi. Zefzafi alikamatwa mwezi Juni mwaka huu na huenda akahukumiwa kifungo cha hadi miaka 20 jela iwapo atapatikana na hatia.
Mji wa Al Hoceima ulio kaskazini mwa Morocco, ni kitovu cha harakati za upinzani dhidi ya serikali. Wanaharakati hao wamekuwa wakisisitiza kuwa, maandamano yao ni muendelezo wa mwamko wa wananchi wa Morocco ulioanza sambamba na mwamko wa watu wa kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati mwaka 2011 na kupelekea madikteta kadhaa kungólewa madarakani.
Serikali ya kifalme ya Morocco imekuwa ikitoa ahadi isizotekeleza za kufanya miradi ya maendeleo katika mji huo, kama wanavyoshinikiza wakazi wake.